Tuesday, September 27, 2005

KITIMTIM KIMEANZA VISIWANI ZANZIBAR

Haya sasa mambo yaliyotokea mwaka 2001 kule visiwani Zanzibar sasa yanatabiriwa kutokea tena kufuatia kuwepo na maneno yanayokinzana miongoni mwa wagombea wa vyama viwili vyenye upinzania mkubwa visiwani huko yaani CCM na chama cha wananchi-Cuf.Bonyeza hapa kusoma habari kamili.

Friday, September 16, 2005

KARIBU SANA MUHIDIN ISSA MICHUZI.

Leo napenda nichukue nafasi hii kumkaribisha rasmi mwanahabari huyu maarufu wa Tanzania ambaye naye amekumbwa na kaugonjwa ka kublogu.Ila yeye amekuja na staili ya aina yake, amekuja na mambo ya mapicha maana yeye taaluma yake hasa ni mpiga picha tena wa siku nyingi sana tangu kipindi cha magazeti ya chama na serikali mpaka sasa kipindi hiki cha utandowazi akh kumradhi utandawazi.Sasa wewe ingia mwenyewe hapa umtembelee na kuzungumza naye mambo mawili matatu.

Sunday, September 11, 2005

ETI TANZANIA NI MAHALI PABAYA SANA KWA KUISHI...

Nashindwa kuelewa hivi hawa wanaojiita watu wa Ulimwengu wa kwanza kama akili zao zipo sawa au wamekomfyuzi kidogo. Hebu bonyeza hapa uone utumbo wanaoongea kuhusu nchi yetu jamani.

Monday, August 08, 2005

WATANZANIA WANALALA NJE CAPE TOWN.

Zamani nilipokuwa bado mtoto mtu akinitajia Afrika kusini nilikuwa najua watu wote wa nchi hiyo ni matajiri.Hata watanzania waliokuwa wakisafiri kuielekea nchi hiyo nilijua tayari maisha yao yameshawanyookea. Baada ya muda pirika za maisha hayohayo zikanifanya niingie katika nchi hiyo ambayo nipo hivi sasa. Ndugu msomaji baada ya kufika hapa nilishangaa kukuta watu walioondoka Tanzania miaka kadhaa iliyopita wakiwa hawana mahali pa kulala katika Jiji hili kubwa lenye baridi kali na la kutisha. Sio kwamba nawacheka hawa watu la hasha, ila maisha yanasikitisha. Kibaya zaidi wapo ambao wameshasahau kwamba wao ni binadamu wamejikita katika uvutaji wa madawa ya kulevya yanayouzwa kwa wingi na makundi ya Wanaijeria walioamua kuharibu maisha ya vijana wenzao waliojidanganya kuja kutafututa maisha Afrika kusini.
Ndugu msomaji endelea kufuatilia yanayojiri katika blogu hii kwani mambo sasa ni kama kawaida.

KIMYA KINGI KINA MSHINDO MKUU... SASA FURAHA IPO PALEPALE

Wahenga walisema kimya kingi kina mshindo mkuu. Mimi binafsi nauamini msemo huu kwani siku zote ukiona kobe kainama ujue anatunga sheria. Kwa kipindi kirefu sasa wapenzi wa blogu hii wamekuwa wakikosa mambo mbalimbali kutokana na kutokuwepo na habari mpya ndani ya blogu waipendayo ya furahia maisha yako. Hii ilitokana na kubadilisha makazi toka katika mji mmoja kuingia katika mji mwingine.Kwa sasa makazi yangu yapo katika Jiji la Cape Town hapa South Africa. Tangu nimefika hapa Cape Town nimekuwa nikikusanya habari na mambo mbali mbali hasa yanayowahusu watu weusi na Watanzania waishio katika Jiji hili lenye kila aina ya starehe, shida, unyama na mambo mengine ambayo nitakufahamisha kwa kina. Nikisema kuna shida hapa kwa wale wenzangu walio Afrika ya Mashariki wananiona nawakejeli lakini huo ndio ukweli wenyewe. Nitakuwa nikiwapa kisa kimoja kimoja ili kukujulisha hali ya maisha hapa Cape Town. Kwa wale watakaopenda kunitumia ujumbe mfupi wa simu au kunipigia namba yangu ni hii +27724696433

Friday, January 28, 2005

MAPAPARAZI WALAZIMISHWA KUPIMA NGOMA KWENYE SEMINA YAO.

Hasira za kuonekana vimbelembele kwa masuala ya wenzao na kunyamazia ya kwao, juzi Jumatano zilsababisha waandishi wa habari 20 kupima UKIMWI.

Waandishi waliochukua uamuzi huo ni wale wa mkoani Arusha waliokuwa wakihudhuria semina ya elimu kuhusu masuala ya UKIMWI waliyoiandaa wao wenyewe kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Arusha.

Kilichowatia hasira waandishi hao mpaka wakapima afya zao ni dongo walilotupiwa na mmoja wa watoa mada katika semina hiyo, Bw. Ezekiel Tuya ambaye aliwashangaa waandishi wa habari kwa uhadari wao wa kuonyesha wenzao vidole wakati yakwao wanayafumbia macho.

Kwa macho makavu kabisa bila ya woga wala haya Bw. Tuya aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanaishangaza sana jamii kwa kupenda kuandika habari za wafanyakazi wa sekta nyingine walioathirika na UKIMWI wakati wenzao walioikumba miwaya hawawatangazi.


Ili kuwatia hasira zaidi, Bw. Tuya aliwaambia waandishi wa habari 25 waliokuwa kwenye semina hiyo kuwa huenda hata wao tayari wameshaikanyaga miwaya alakini kwa sababu hawajapima ndio maana hawajijui.

Kutokana na hasira walizopata kwa kutupiwa madongo hayo, waandishi 20 waliamua kupima afya zao bila ya hiyari na wenzao watano waliobaki waliendelea kuwa ngangari katika suala la kupima.

Baada ya zoezi hilo, Mwenyekiti wa Klabu hiyo Bw. Ulimboka Mwakili alisema changamoto waliyopewa na Bw. Tuya ni ya maana na itakuwa changamoto ya wao kuwahimiza waandishi wenzao wa habari nchini kupima afya zao.




KITABU CHA WAGENI YAANI GESTI BUKU KINAANDALIWA

Wapenzi wasomaji kile kitabu cha wageni kwa ajili ya kujiorodhesha kwenye blogu hii maridhawa kwa ajili ya kutoa maoni au ushauri sasa kipo mbioni kukamilika.Nawashukuru sana wale wote ambao wamekuwa wakiitembelea blogu hii mara kwa mara kwa lengo la kujifunza na kuburudika naomba tuendelee kuonyesha mshikamano kwa sababu mambo ya mwaka huu si ya kawaida.Kwa wale wanaotembelea blogu hii sasa hivi tafadhali naomba mnapotoa maoni yenu kama wewe sio mwanachama na unatumia anonymous jitahidi kuweka email yako ili tuweze kuwasiliana na wewe kama kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
ASANTENI NA NINAWATAKIA SIKU NJEMA

Friday, January 21, 2005

INAKUAJE MNALILIA NGONO MKIPEWA MNASAHAU KUVAA CONDOM MTAKUFA!!!

Mkipewa vaeni kondomu
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Frederick Sumaye, ameshangaa inakuwaje mijitu mzima mingine inapenda ngono mpaka inalilia, lakini ikipewa inasahau kuvaa kondomu.

Kitu kingine kilichimuacha hoi Waziri Mkuu ni kwamba; wakati mijitu hiyo inapokubaliwa kupewa, inakuwa na jitihada za hali ya juu sana ya kutoa pesa nyingi za kukodisha chumba gesti na hata kwenye hoteli za bei mbaya, ila kununua kondomu ya Sh. 100 tu inakuwa kasheshe!

Yaani wanashangaza kweli kweli. Utaona mtu mzima, anafahamu kuwa kuna UKIWMI... analipia kitanda, lakini hata kondomu havai, wengine wanadiriki kulilia ngono! alishangaa Mhe. Sumaye kwenye mkutano wa hadhara kule Shinyanga.

Kinachomuacha hoi zaidi Mhe. Sumaye ni kuwa wengi wanaofanya hivyo ni wale waliomahodari sana kwenda misikitini na makanisa wakijitia waumini wazuri wanaosikiliza mahubiri ya masheikh, wachungaji na mapadre.

Sasa mbona maaskofu na masheikh wamehubiri juu ya Ukimwi lakini bado watu hawaelewi na badala yake wanaendekeza ngono zisizo salama na ambazo ni hatari kwa maisha, aliwasuta.

Alisema; kuna watu wanaodhani kuwa kufanya ngono ni sifa, watakufa na kama mtu anashindwa kujizuia ni bora akafanya ngono salama kwa kutumia kondomu.





Wednesday, January 19, 2005

JAMANI MNAOVAA TAI NA SUTI MNAZIJUA SHERIA HIZI.

Vazi la suti mara nyingi humfanya mvaajia aonekane nadhifu na mwenye heshima ndani ya jamii anayoishi hususani kwa akina baba kabwela. Pia kuna uvaaji wa suruali nyepesi, shati jepesi, kiatu cha mchongoko na tai inatangulia mbele watoto wa Dar wanasema vazi la "kipapaa". Vazi hili kutokana na heshima lukuki linazopata kutoka kwa jamii hasa ya makabwela kama nilivyokwisha kusema awali limekuwa likitumika hata na wahalifu kama majambazi na matapeli katika kuwalaghai watu mbalimbali ambao ndio huwa walengwa wa uhalifu wao. Pia vazi hili hupendelewa kutumiwa na viongozi, na mabwana harusi au hata wakurugenzi na mabosi wa mashirika, taasisi, na makampuni mbalimbali.
Lengo langu siku ya leo ni kuwaleteeni sheria zinazotakiwa kuzifuata mtu anapovaa suti la sivyo unaweza kujikuta upo matatani kwa kuvunja moja ya sheria hizo. Sheria zenyewe ni kama ifuatavyo. Unapovaa suti au tai hakikisha huvunji sheria hizi hapa chini:-
1. Ni marufuku kuvaa kandambili au malapa
2. Ni marufuku kuvaa soksi mbovu.
3. Ni marufuku kujisaidia uchochoroni.
4. Ni marufuku kupenga kamasi barabarani.
5. Ni marufuku kupanda daladala.
6. Ni marufuku kuendesha baiskeli au pikipiki.
7. Ni marufuku kucheka cheka hovyo.
8. Ni marufuku kuomba change dukani.
9. Ni marufuku kubeba mfuko wa plastiki maarufu kama rambo
10. Ni marufuku kuingia kwenye kibanda cha simu.
11. Ni marufuku kula magengeni.
12. Ni marufuku kuonekana unatafuna barabarani.
13. Ni marufuku kutembea na pesa za sarafu mifukoni mwako.
12. Ni marufuku kulia hata kama umeletewa taarifa ya msiba.
14. Ni marufuku kupiga miruzi.
15. Ni marufuku kuonekana unatoka mijasho kama unasukuma mkokoteni.
16. Ni marufuku kuongea kwa kelele.
17. Ni marufuku kunywa chai au kahawa kwa kutumia kikombe cha plastiki.
18. Ni marufuku kutembea kwa miguu.
19. Ni marufuku kukimbia.
20. Ni marufuku kunuka mdomo wala kikwapa hili kosa kubwa sana na hukumu yake mpaka mbinguni ipo.
21. Ni marufuku kusema uongo.
22. Ni marufuku kuonekana umekasirika unatakiwa uwe na uso uliokunjuka.
23. Ni marufuku kumchapa mtoto.
24. Ni marufuku kusababisha ubishi au mjadala uso na maana.

Kwa leo tuanamaliza na sheria za suti na tai siku nyingine tutawaletea masharti ya kujiunga na chuo na vibaka huko maeneo ya uwanja wa fisi jijini Dsm.